Moja ya shauku kubwa kwa watu wengi ni kuwa na maisha yaliyo salama na mazuri yenye utoshelevu wa mahitaji yao.
Unahitaji kujua ni uchaguzi wako kuyaweka maisha yako katika sehemu salama au si salama.
Unaweza kuwa katika mtihani mkubwa pindi unapowekewa vitu hivi viwili mbele yako ili uweze kuchagua kati ya usalama na ustawi, kwani kuna maisha yaliyo salama lakini hayana ustawi inakuwa teso, pia unapokuwa na ustawi pasipo na usalama basi hapo mashaka na hofu vita tawala na kupelekea hata kushindwa kuona fahari ya ustawi wako.
Lakini hivi vyote viwili vikiwepo ( ustawi na usalama ) hapo maisha yanaweza kuanza kama sio kuyafurahia.
Moja ya ombi la watu wengi katika dunia ya sasa ni kuweka maisha yao katika mikono ya Mungu, wengi wamefikia maamuzi hayo baada ya kuweka imani kwa watu/vitu na kutopata matokeo yastahiliyo / waliyo yategemea hivyo wamerudisha imani yao ya kufikirika kwa Mungu.
Wako walioweka matumaini yao katika kazi na kazi ilipoisha walijikuta katika mazingira magumu sana, pia walioweka maisha yao mikononi wa wenzi wao lakini mwisho wake wakajikuta wako nchi kavu badala ya kuwa majini kama samaki.
Pia wako watu wengine wamekuwa wakiamini kwa kuombewa na watu wenye majina au watumishi wa Mungu wanaojulikana itasaidia maisha yao kuyaweka katika mikono ya Mungu na wengine wamekuwa tayari kutoa kiasi chochote cha fedha ili mradi tu maisha yao yawe mikono mwa Mungu kupitia fedha zao.
Matendo 8:20 Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.
Unahitaji kujua maisha yako kuwa katika mikono ya Mungu ni shauku ya Mungu mwenyewe, hivyo ukimwelewa tu utampata na kupata usalama wake.
kila kitu ili ukipate unahitaji kujua utaratibu wake ili kiwe chako.
1 Nyakati 28:9 Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.
Unahitaji kujua maisha yako kuwa mikononi mwa Mungu ni matokeo ya KUMPENDA MUNGU TU, na sio kitu kingine chochote.
Unahitaji umpende ili maisha yako yawe maisha yake ( yeye aishi kupitia wewe ).
Hauhitaji kumshawishi Mungu ili maisha yako yawe mikononi mwake, yeye sio kuku ukitaka kumkamata basi umwage mahindi ndipo umkamate na kumchinja.
Moja ya ishara ya kumpenda Mungu ni hali ya juu ya kumtaka kumsikia yeye kuliko chochote: wewe binafsi, mali au kitu chochote.
Marko 10:17 Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?
18 Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.
19 Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.
20 Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.
21 Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.
22 Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
Kuna tofauti kubwa kati ya kumpenda Mungu na kuwapenda watu/ mtu kwa upande wa mtu ni vigumu kujua kinachoendelea katika moyo wake japo kinaweza kuwa ni chema au kibaya bado usijue mpaka matokeo ya tokee lakini Mungu anajua hata mawazo ya moyo wako hata kabla ujatenda.
- Kwahiyo kwa Mungu anajua unampenda hata kabla hujasema unampenda.
Mwanzo 4:6 Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.
Ni kweli moja ya ishara ya kumpenda Mungu kuhudhuria nyumba za ibada lakini hiyo sio ukamilifu wa kumpenda Mungu kwa kuwa unaweza kuwa mhudhuriaji mzuri kanisani lakini ukawa una lengo lako tofauti na ibada.
Ni muhimu ujue kunatofauti kati ya kuwa kanisani na kuwa ibadani, ili ibada yako iwe na maana ni lazima moyo wako umbebe Mungu kwa ukamilifu wake na sio matatizo.
Japo kwa uhalisia ni ngumu kujua maslahi ya mtu anayekuja kanisani huo utumishi umebebwa na nini?
Mathayo 7:16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
Mungu si mwanadamu hivyo unapoamua kumpenda Mungu basi hakikisha unampenda kwa uhalisia wake, ( umpende vile unavyotaka umpende ).
Ni Mungu tu anayeweza kukupenda katika hali zote pale utakapoamua kumpenda sasa na milele.
huwa hatumpendi Mungu kutokea hewani bali katika kumjua yeye na pendo lake vile lilivyo.
Ukimjua Mungu hauwezi kuacha kumpenda na ukimpenda naye atayachukua maisha yako na kuyaweka mikononi mwake hata bila kuomba sana.
“ ukimpenda atakupenda”
“ukimfurahisha naye atakufurahisha”
INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA
Imeandaliwa na:
Cothey Nelson……………………………………….………………………………………..0764 018535