Hakuna kitu kizuri kama mtu kukuona vile ulivyo!
Maana ni hatari sana mtu kukuona nje ya uhalisia wako, unaweza kuishi maisha ya mateso bila kutarajia na ukajikuta umeingia humo bila kutaka.
Mathalani unaweza kukuta umetoka na wenzako na mkiwa sehemu ya kupata vinywaji, ki ukweli unaweza kuwa ulikuwa na uhitaji wa kunywa soda lakini ukakuta rafiki zako wote wanakunywa maji, hivyo nawe ukaagiza maji badala ya soda na hali hiyo ikapelekea kunywa maji pasipo kuyafurahia, ukanywa maji utafikiri unakunywa dawa yenye uchungu uliopitiliza.
Naam pia unaweza kuulizwa kuwa unajua kuendesha gari? Nawe kwa kuona usimwangushe yeye aliye kuuliza ukamwambia unaweza lakini ukweli unajua huna uwezo mzuri wa kulimudu gari! Lakini mwishowe unaweza pata madhara makubwa hata ikapelekea kujuta na kujilaumu kwamba ni vyema ungesema ukweli tu ungekuwa salama kuliko kuisababishia hasara kubwa taasisi husika.
Pasipo kujua unapokuwa wazi unakuwa ni rahisi kusaidika kuliko kutokuwa wazi maana unaweza usisaidike au ukachelewa kusaidika.
Unapotambua uhalisia wako ( vile ulivyo ) unampa urahisi hata mtu anayetembea na wewe mathalani unapotembea na mtu ukajua anashida ya miguu bila shaka utatembea na yeye kwa taadhari kubwa huku ukihakikisha ufanyiki teso juu ya huyo ndugu lakini ukakuta mtu ni anashida ya miguu lakini anataka usijue kuwa yeye anashida hiyo nawe ukatembea naye kama mtu asiye mdhaifu wa miguu naye akajitahidi kama mtu aliyemzima kabisa bila shaka ikitokea amemaliza salama safari yake atakuwa na maumivu makali sana na inaweza kupelekea hali yake kuwa mbaya zaidi kuliko awali.
Mtu kukujua vile ulivyo ni ishara ya utayari wa dhati na usiyependa kumsumbua katika safari yake.
Ndivyo hivyo hata kwa upande wa Mungu…………….
Usitafute Mungu kukuona kama watu wanavyokuona utapata shida na unaweza kujikuta unafurahia kitu ambacho hakifurahishi.
Usitake kuona kama Mungu ameona umevaa wigi la gharama kiasi gani? Nguo kiwango gani?, Ukienda kwa Mungu kwa jinsi hiyo bila shaka kuna kipindi kitafika utataka Mungu akuabudu badala ya wewe kumwabudu Mungu.
Mungu haitaji sana kuona maendeleo yako ya mwilini japo wewe uweza kujifurahia lakini hasa anahitaji kuona maendeleo ya roho yako.
Unahitaji kuwa mbele za Mungu vile ulivyo maana yeye anakujua vizuri zaidi sana, na maana wewe kuwa vile ulivyo mbele za Mungu ni ishara kubwa kuwa uko tayari yeye Mungu kufanyika kuwa utoshelevu wako na stara yako.
“ Isaya alipogundua midomo yake michafu”
Isaya 6:5 Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.
6 Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;
7 akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.
8 Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.
9 Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione.
10 Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa.
Japo alikuwa nabii mkubwa anayeaminika lakini alienda mbele za Mungu na kujidhiri vile alivyo na kuonyesha uhalisia wake mbele za Mungu naye Mungu akatakasa kinywa chake ili kizidi kufaa.
INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA
Imeandaliwa na:
Cothey Nelson……………………………………………………………………………………….0764 018535
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni