Ijumaa, 1 Agosti 2025

ISHI KATIKA JICHO LA MUNGU

 



Katika jicho la Mungu hapo ndipo kuna umilele wako.

Hivyo unavyoishi hapo basi ujue unaishi katika asili yako na uhalisia wako.

Ni hali ya kawaida na ya wazi ili uweze kuwa kivutio kwa mtu fulani ni lazima uweze kuleta ushawishi katika macho yake yaliyobebwa na maarifa/ufahamu wa Mungu juu ya jambo hilo.

Ni kweli kila jicho la mtu litakavyo kuona litatoa tafsiri yake juu ya muonekano wako, wanaweza kuwa watu watano (5) , lakini inawezekana wawili wakakuona umependeza na wengine wakakuona hujapendeza.

Hivyo mtu mmoja unaweza kuwa na tafsiri nyingi kutoka kwa watu wanaokutazama kutokana na mtazamo wao juu yako.

Hivyo mmoja anavyokwaambia umependeza sio wote watakao kwambia umependeza haijalishi nguo umennunua kiasi gani?

Moja katika janga kubwa hapa duniani ni kufanya kitu  ili KUFURAHISHA WATU au WATU WAKUKUBALI au WAKUPENDE.

Huu ni moja ya mtihani mgumu sana katika dunia ya leo, kwakuwa tendo lako moja linaweza beba tafsiri zaidi ya elfu moja kwa watu unao wafanyia na zingine zinaweza kuwa mbaya na zingine zinaweza kuwa nzuri.

Maana unawezafanya kitu sahihi na chema kwa watu na bado wasione huo wema.

Ndomana unaweza kukuta mtu anajigharamu sana kuhakikisha rafiki yake au mpenzi wake kuwa katika mazingira mazuri yatakayofanya  yeye afurahie maisha yako na kuongeza upendo kwako, lakini unaweza kukuta wewe unafanya wema lakini yeye hatafsiri kama wema anaweza kutafsiri kama unajipendekeza au unapoteza muda ambao baadaye utakuja kujutia.

Kumbuka unapofanya wema kwa mtu huwa cha umuhimu ni hile tafsiri ya moyo wa mpokeaji na sio ukubwa au udogo wa jambo unalomfanyia.

Watu wengi wamejikuta katika kuhakikisha dunia inawafurahia pasipo kuangalia jicho la Mungu linawatazamaje?

Wako watu waliokuwa wazi wa kumfurahisha rafiki ,boss, ndugu ama wazazi lakini wamkose Mungu kwa kujua au kutokujua.

Na inapotokea huo wema unalipwa katika ubaya wakati wewe ulitegemea dunia itathamini wema wako lakini imekuwa tofauti bila shaka unaweza kujuta hata kwanini ulifanya huo wema.

Lakini pindi utakapofanya wema ukilenga kupata kibali katika jicho la Mungu bila shaka utapata malipo zaidi ya ule wema ulioufanya kwa watu haijalishi hao watu wameupokeaje?

Unapaswa kujua jicho la Mungu linapokuangalia katika wema unaoufanya kwa mtu au watu basi hapo unakuwa mahali sahihi.

Unapoishi katika jicho la Mungu unapata neema ya kutambulishwa na kuelekezwa ni nani umfanyie huo wema ili uwe msaada wa kudumu katika maisha yake.

Kumbuka wema unalipwa na Mungu na sio watu, hivyo wema unaoufanya kwa watu usitegemee malipo kutoka kwao hata kama watafanikiwa.

 

INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA.

 

Imeandaliwa na:

 

Cothey  Nelson …………………………………………………………………… 0764 018535

Ijumaa, 18 Julai 2025

AKILI NJEMA

 



Akili njema ni zaidi ya akili yenye afya!

Ni akili isiyobeba lawama juu ya mtu yeyote, kuwa ndiye kikwazo katika maisha yake.

Bali ujiona yeye ndiye chanzo cha kwenda mbele au kurudi nyuma.

Akili njema mara zote ufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi ( utembea katika hekima ).

Pia hii akili haina kukata tamaa wala kuchoka maana huona hali yoyote ya kushindwa kufanikisha jambo, yeye ndio muhusika wa kushindwa kukamilisha na wala sio mtu mwingine wa kulaumiwa nje ya yeye.

Akili njema utegemea sana chakula gani unakula ili kuilisha akili yako, maana ukila chakula kisichokuwa bora inaweza pelekea akili yako kukosa afya njema na kupelekea kushindwa kufanya lile unalopaswa kulifanya kwa ukamilifu.

Ikumbukwe kuwa kuna tofauti kati ya chakula cha mwili na chakula cha akili, chochote kinachoongeza tija katika ufahamu wako basi hicho ni chakula cha akili na chochote kinachoongeza tija katika mwili wako basi ni chakula cha mwili, japo kuna wakati chakula cha mwili kinaweza kuwa na tija katika ufahamu wako/akili yako.

Akili hii upelekea kuwa na hali ya kujitegemea au kijisimamia mwenyewe haigemei kwa mtu yeyote!

Maamuzi yanayotokana na akili hii siku zote yanakuwa thabiti yenye nia njema isiyobebwa na mashindano.

Unahitaji kuwa na akili njema ili kuona yasiyowezekana kuwa yanawezekana maana akili njema uwa inatoa mwanga palipo na giza.

Na hili uweze kumtegemea Mungu katika viwango vyake ni lazima uwe na akili safi/njema.

Nini maana ya akili njema?

i. Ni hali ya kujitambua na kusimamia yale unayopaswa kuyafanya kwa uaminifu.

- Unapaswa kujitambua wewe kuwa una majukumu tayari na wewe ndio muhusika kufanikisha hayo majukumu, na unahitaji akili njema ili uweze kufanikisha yale unayopaswa kufanya.

Unapaswa kuyasimamia majukumu yako kutoka kwenye akili yako iliyo njema pasipo kuwa tegemezi popote.

ii. Ni hali ya akili yako kumuhusisha Mungu kwa asilimia mia moja katika utendaji.

- Kuna wakati akili yako inakosa majibu kwa namna yake, kwasababu inamipaka hivyo kushindwa kutoa jibu linalopaswa.

Hapa Mungu anaitengeneza akili yako katika akili yake na kufanya yale yaliyoshindikana kutoka kwenye akili yako.

Na hapa ndipo Mungu ufanya ili kuleta maajabu ya mbingu hapa duniani ili kuutangaza ufalme wake.

Unahitaji kumsikiliza sana Mungu katika utulivu na utayari ili paweze kuleta wepesi wa akili yako kuielewa akili ya Mungu hivyo kupelekea utendaji wake kufanikiwa.

Unapaswa kuuelewa utendaji wa Mungu ili uweze kuuruhusu kuwa na nafasi katika akili yako.

Unapokuwa na akili njema hata mwili wako unaweza kuwa na afya njema, maana kuna baadhi ya magonjwa yanazaliwa pale akili yako inapokosa majibu au utatuzi uliosahihi mathalani magonjwa ya pressure au kupalalaizi ( stroke ) yanaweza kuathiri mifumo ya mwili wako na kufanya kuwa dhaifu.

Usipopambana kuwa na akili njema bila shaka utaishi katika akili mbaya.

 

INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA

 

Imeandaliwa na:

 

Cothey Nelson ……………………………………………………………………………………0764 018535

 

Ijumaa, 4 Julai 2025

AKIKUONGOZA UTAKUWA SALAMA

 



Kuongozwa ni jambo la uhiyari!

Na uwa hatufurahi kwasababu tunaongozwa tu bali tuna furahi kwasababu anayetuongoza anaijua njia na katika maongozi yake usalama unaambatana na wewe,

Ni rahisi kwa njia isiyo na maporomoko mengi kuona kuwa kuna uwezekano wa kufika unakoelekea lakini endapo utakuta kuna njia sio rafiki bila shaka wasiwasi utakuwa na sehemu yake ndani yako.

Haupaswi kuogopa mazingira yasiyo kuwa rafiki ukaona kuwa haufiki bali hakikisha tu unapata maongozi yaliyo sahihi ili ikuweza kupita salama katika mazingira yasiyokuwa rafiki, Ni kama vile unavyoona giza lililozito haupaswi kuliogopa hilo giza lakini hapo ili uwe salama ujue unahitaji mwanga ( maana mwanga ni mbabe wa giza ).

Unaweza kuwa na kitu kizuri ama nafasi nzuri lakini ikatokea ukakosa mwelekeo sahihi unaweza ukajikuta unapoteza ule uzuri au nafasi uliyonayo, mathalani wastaafu wanaopata kiinua mgongo chao au mafao yao endapo wasipopata mwelekeo sahihi ya hizo fedha uweza kujikuta wanapoteza fedha zao na kupelekea kuishi maisha ya majuto na kuruhusu magonjwa yaanze kushamiri ndani ya miili yao.

Kama binadamu uliye na pumzi ya Mungu maadamu unaishi basi kuna mahali unaelekea, mbali katika hali ya ukuaji utoto kwenda ukubwani pia kuna maisha unayoishi sawasawa na ndoto uliyonayo wewe binafsi au ndoto ya familia yako.

Hivyo unahitaji maongozi sahihi ili uweze kufika sehemu sahihi, hivyo ukikosa maongozi sahihi ni vigumu kutimiza lengo katika safari yako.

Roho mtakatifu ni kiongozi pekee aliyebeba usalama wako kwa ajili yako.

Huyo Roho anajua mifumo yote ya dunia na usiri uliojificha ndani ya moyo wa mwanadamu hakuna asichokijua au kilicho kificho katika yeye.

Nje ya yeye usalama ni mdogo sana haijalishi nini kinaonekana kuwa kina usalama basi jua usalama huo sio wa kudumu.

“ Roho atawafundisha na kuwaongoza………….”

 Yohana 16:13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Unahitaji kuokoka ili uweze kumpa nafasi aweze kuchukua madhaifu yako au kuchoka kwako na yeye akupe uimara wake na nguvu zake.

Ni kweli mtu anaweza kuajiriwa na kupewa mshahara mzuri sana lakini anaweza asione wapi anaelekea na kesho yake ni ipi?

Na wakati mwingine unaweza kuwa na mipango mizuri kutokana na kipato chako lakini ukashindwa kuyafanya hayo kuwa hai kutokana na hali ya uzito ya kuchukua hatua au vipingamizi unavyo viona.

Pia unaweza fanya kazi binafsi au kuajiriwa ukajikuta moyo wako ni mzito umechoka kabisa na hata ukakosa muelekeo lakini pindi utakapopata  muelekeo sahihi wa Roho mtakatifu unaweza kutoka hapo katika hali ya kushindwa na kuwa mshindi.

 

Yakupasa kujua maongozi sahihi ni afya ya maisha yako.

 

INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA

 

Imeandaliwa na:

 

Cothey Nelson …………………………………………………………………………….0764 018535