Ijumaa, 17 Januari 2025

KAA KATIKA KITI CHAKO.

 


Moja ya kitu kizuri ni kukaa sehemu uliyoandaliwa kukaa, na sio sehemu unayoitaka wewe kukaa.

Unapokaa sehemu unayopaswa kukaa bila shaka kuna faida nyingi zitaelekezwa hapo kwa kutambua sehemu hiyo imekaliwa na mtu husika.

Wakati mwingine unaweza kutamani kukaa katika kiti ambacho sio chako / haujaandaliwa wewe japo kinaweza kuwa katika eneo zuri ambalo watu wengi wakiangalia hapo wangekuona wewe basi nawe ungejisikia vizuri.

Unapokaa mahali au sehemu sio yako ama hujapangiwa bila shaka unaweza kupata mambo usiyotarajia kwa kuwa umekaa sehemu isiyo yako baada ya kupafurahia ukakuta unaboreka.

Mathalani unapokaa sehemu sio yako unaweza kukuta wewe ni mnywaji wa soda unaweza kuletewa bia, unaweza kuona wamekudharau au wamekuonaje?

Pia katika hali ya kawaida unaweza kujikuta umechoka kukaa katika sehemu moja kwa muda mrefu hali ya hewa inaweza kubadilika mathalani kuna wakati inaweza kuwa mvua au jua ukatamani kuhamia upande mwingine unaweza kujikuta umeshindwa kurudi upande ulipokuwa umekaa hapo awali.

Kila mahali  pana ukaaji wake msibani au harusini  huwa kuna utaratibu wake kila sehemu kuna wahusika wake mathalani huwezi kuingia katika harusi alafu ukakaa mahali bibi harusi anakaa na we ukatulia tuli na kuanza kuperuzi mtandaoni kwenye simu yako na amani tele na hata watu wakiingia wewe bado umekaa tu utafikiri mpambaji.

Ni muhimu utamani na ufurahie kukaa katika kiti chako/ sehemu yako.

Kwasababu kuna baadhi ya mambo unaweza kuyakosa kwa kukosa kukaa sehemu uliyopaswa kukaa.

Yakupasa kujua kuwa sehemu yako tu, ndio iliyobeba ustawi wako na Mungu anakusudi kamili la wewe kukuweka hapo haijalishi hayo mazingira yanaonekanaje au yanatoa mtazamo gani kwa mtu au kwa watu.

Unapaswa kujua Mungu anapokuweka hapo ana kuandaa kwa ajili ya utukufu wake maana wewe umetokana na yeye.

Ni muhimu utambue sehemu yako ni ipi popote ulipo ili ufanye kwa ufanisi mkubwa maana unaweza kujikuta unatembea katika maeneo ya wengine na kuwasaidia huku sehemu yako ikibaki kama ilivyo pasipo kufanyiwa kazi yoyote.

Pia ni vizuri utambue kuwa sisi kama mwili katika kristo ni viungo kila mmoja kwa mwenzake, katika mwili wa binadamu kazi ya jicho haiwezi kufanywa na mkono hivyo tambua unaposimama kama jicho basi hapo unakuwa mwanga na usaidizi katika mkono katika kuendelea na majukumu yake pia unaleta ladha na mng’ao wa tofauti na tija katika mwili wote, maana viungo katika mwili wa binadamu vinahitajiana ili mwili uweze kufanya kazi yake katika hali ya ubora.

Ni lazima utamani kukaa katika kiti chako ili uweze kupata mema ya mbingu na sio mema ya dunia kwa kitambo.

Bila shaka unapofurahia kiti chako na kukaa kwa kutulia mbele za Mungu utapelekea watu waone ukuu wa Mungu kupitia wewe.

 

INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA

Imeandaliwa na:

Cothey  Nelson………………………………………………………………………0764 018535

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni