Jumamosi, 1 Juni 2024

AKILI YA MUNGU:



Akili ndio kitu pekee kinachomtambulisha mtu kwa ufasaha zaidi, unapomuangalia na kuona namna anavyofanya mambo yake unaweza kugundua uwezo wa akili yake au mapana au ufinyu wa akili yake!

Unapokuwa na akili ya Mungu unakuwa na neema ya kufanya mambo ambayo akili ya kuzaliwa imeshindwa kutoa matokeo sahihi.

Ni dhana ya kawaida sana, ina aminika kwa asilimia kubwa ili uweze kuufurahisha moyo wa mtu lazima ufanye kitu kinachoendelea kwenye akili yake haijalishi ni kidogo au kikubwa.

Ukifanya kitu ambacho  hakizunguki kwenye akili ya mtu sio rahisi kugusa moyo wa mtu huyo, hata ukifanya kwa ustadi gani au kwa muda wa kutosha kiasi gani bado hautaweza kuleta ushawishi kwa mtu husika.

Naam njia rahisi ya kuwa kitu chochote basi pata/ kuwa na akili yake, mathalani unapokuwa na akili za mnyama basi utafanya matendo ya mnyama, vivyo hivyo unapokuwa na akili ya wadudu basi nawe utakuwa mdudu japo kwa muonekano utaonekana ni binadamu lakini matendo yako yatadhihirisha akili iliyo beba wadudu.

-          Ndio maana kuna matendo binadamu akifanya watu utakuta wanasema “ wewe sio binadamu bali ni mnyama……maana hauwezi kufanya ukatiri mkubwa kiasi hiki “

Kwa kusema hivyo sina maana kwamba kila atendalo mnyama, ndege au mdudu halifai kuigwa au kupata funzo kutoka kwao. La hasha! Yako matendo mengine ya myama au ndege ni mazuri hata kuliko ya wanadamu mathalani hauwezi kuona jogoo kampanda jogoo mwenzake lakini binadamu unaweza kukuta mwanaume anamuoa mwanaume mwenzake na kuishi kama mke na mume kitu ambacho huwezi kukuta kinafanyika kwa wanyama au ndege hata wadudu.

Sio hilo tu pia kuna ndege kama vile kuku anatabia ya kupigania vifaranga vyake kwa gharama yoyote inawezekana yuko radhi yeye asile vizuri lakini ahakikishe vifaranga vyake vimekula vizuri na hata ikitokea kifaranga kimeumia yuko tayari akae hapo kwa muda wote maadamu kifaranga chake kinahitaji uwepo wake, lakini sio baadhi ya wazazi hasa wanaume huweza kutelekeza familia zao kutokana na sababu mbalimbali na kuiacha familia wakati familia inategemea uwepo wake ili maisha yaende.

Moja ya kitu kinachoweza kukusaidia kukaa na mtu yeyote awe kichaa, mwendawazimu, mshirikina, mwizi au kibaka ni uwezo ulionao katika kutambua kinachoendelea katika akili yake na kuwa tayari kukibeba kwa upendo wa dhati pasipo kuangalia gharama yake.

Naam na hata katika dunia ya sasa neno ugonjwa wa akili limekuwa na mdahalo mkubwa katika kutafuta muafaka wake, watu wengi wamekuwa wakichukua maamuzi ya kujiua au kujichukia kwasababu ya mambo wanayo ya kabili yaliyo kosa majibu katika akili zao.

Unahitaji akili yako kuwa salama ili maisha yako yawe salama na pindi akili yako ikishindwa kung’amua fumbo linalo kukabili basi ujue hapo maisha ya mateso yanakuwa ni fungu lako.

Na akili yako ikiwa kifungoni basi hapo ujue na maisha yako yako kifungoni.

Na moja ya msaada mkubwa unaoweza kumpatia mtu mbali na hitaji la haraka alilonalo ni kumpa mtu majibu katika maswali yanayoendelea katika akili yake.

Na mara zote pindi akili inapokosa majibu inamfanya mtu ashindwe kwenda mbele au kurudi nyuma maana anaona mbele hapawezekani na wakati mwingine hata nyuma anaona haiwezekani tena ni kama mbwa kurudia matapishi yake.

Kwa kiasi kikubwa ukichunguza vizuri utendaji wa akili yako unaweza kupunguza lawama juu ya watu unaoweza kuwaona wamechangia matatizo yako.

“ unahitaji akili ya Mungu ili uyafanye yaliyo ya Mungu “

Unapotembea katika akili ya mtu unakuwa wewe umemvaa huyo mtu wakikuona wewe wana muona yeye anayetembea katika akili zako.

Hivyo unavyotembea katika akili ya Mungu watu wanamuona Mungu akitatua shida zao na kuwapa mwelekeo uliobora.

Katika akili ya Mungu kuna uhai na nguvu kupitia neno la Mungu ambalo linafanya akili yako iwe kama Mungu alivyo.

Unapaswa kujua ustawi wako unabebwa katika akili ya Mungu, kwa kutembea katika akili ya Mungu hauwezi kuchoka wala kukata tamaa.

Na sikuzote akili ya Mungu inatembea katika kalenda ya mbingu na sio ya wanadamu au kalenda ya dunia.

Ishi kwenye akili yake uone maajabu yake!

INAITWA SIKU! BARIKIWA SANA

Imeandaliwa na;

Cothey  Nelson ……………………………………………………………………………………………….0764 018535

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni